Mkuu wa Kurugenzi ya Mifumo ya Uchaguzi Tume ya Uchaguzi Zanzibar Bi. Mwanakombo Machano Abuu amewataka wafanyakazi waliochaguliwa kuandikisha Wapiga Kura Wapya katika Daftari la Kudumu linalotarajiwa kuanza tarehe 2 Disemba 2023 kuhakikisha kila mwenye sifa ya kuandikishwa anaandikishwa na kuachana na ushabiki wa Kisiasa kwani zoezi hilo halihitaji ushabiki wa kisiasa.
Hayo aliyasema huko kwenye Ukumbi wa kiwanda cha Mafuta ya Makonyo Wawi alipokuwa akizungumza na Wakuu wa vituo vya Uandikishaji na Makarani wa Uandikishaji waliochaguliwa kwa zoezi hilo.
Alisema Uandikishaji utaanzia katika Wilaya ya Micheweni hivyo aliwataka kila mmoja kuelekeza akili yake katika kazi hio muhimu ya taifa kwa kuzingatia uadilifu na kumpa kila mwenye haki yake ya kuandikishwa aandikishwe ili awe miongoni mwa Wazanzibar watakaokuwa Wapiga Kura kwa kuwemo ndani ya daftari hilo la Kudumu la Wapiga Kura.
Alisema “Niwaombe sana jiepusheni na kushabikia vyama wakati wa Uandikishaji kwani kufanya hivyo kunaweza kulitia dosari zoezi zima la Uandikishaji”
Alisema kuhakikisha wanafanya kazi vizuri kwenye zoezi la Uandikishaji huo ni vyema pia kutii maagizo waliyopewa na kujitahidi kutunza vifaa,kufanya kazi kwa siri na kujenga nidhamu itakayoweza kuwasaidia kufanya kazi pasina misuguano baina yao na kulitumikia taifa kwa uweledi katika kazi hio.
Alisema haitapendeza kumuona Karani wa Uandikishaji anatumia VRD nje ya malengo yanayokusudiwa kwani vifaa hivyo vinahitaji kutumika kwa uangalifu mkubwa “naomba nitumie fursa hii kwa mara nyengine tena kuwakumbusha kuwa mnakwenda kufanya kazikatika jamii tofauti kwenu nikuhakikisha mnatoa huduma bora ilisisi tuliokutumeni tuweze kujifariji.
Bi. Mwanakombo aliwasihi kuwa kuwasimamia vyema watu wenye mahitaji maalum kama vile wazee , watu wenye ulemavu au mama wajawazito ili nao waweze kupata haki yao hio bila ya usumbufu.
Nae Afisa wa Uandikishaji Tume ya Uchaguzi Zanzibar Wilaya Chakechake Abdalla Juma Abdalla aliwataka Waandikishaji hao kujenga mashirikiano mazuri na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ili kufanikisha zoezi hilo.
Tume ya uchaguzi Zanzibar inatarajia kuanza zoezi la kuandikisha Wapiga Kura Wapya tarehe 2 Disemba 2023 katika Wilaya ya Micheweni ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi Mkuu wa 2025.