Tume ya Uchaguzi ya  Zanzibar (ZEC), imeandikisha jumla ya Wapiga Kura Wapya wapatao 57,883 katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa awamu ya kwanza. 

 

 Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe.Jaji George J. Kazi alipofungua Mkutano wa Tathmini ya Uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya kwa awamu ya kwanza, uliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini. 

Alisema kuwa miongoni mwa hao walioandikishwa wanawake ni 31,440 na wanaume ni 26,443  huku Watu Wenye Ulemavu walioandikishwa ni 1,280.

Aidha, alisema kuwa hatua ya Uandikishaji imekamilika na Tume inatarajia kuweka wazi orodha  ya Wapiga Kura hao katika vituo vyote vilivyotumika kwa Uandikishaji wa Unguja na Pemba kwa muda wa siku saba kuanzia  Machi 1 hadi 7 mwaka huu. 

Alifahamisha kwamba kazi hiyo inafanyika kwa mujibu wa maelekezo ya kifungu cha 19(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar namba 4 ya mwaka 2018 , ambacho kinamtaka Afisa wa Uandikishaji, kutayarisha na kuweka wazi orodha ya Wapiga Kura walioandikishwa kwa muda wa siku hizo katika eneo la wazi la Afisi ya Wilaya au eneo jengine lolote litakaloamuliwa na Tume. 

Aidha alisema sambamba na uwekaji wa wazi wa orodha ya Wapiga Kura Wapya, Tume itaweka wazi orodha ya Wapiga Kura walioomba kuhamisha taarifa zao kutoka eneo moja kwenda eneo jengine la Uchaguzi. 

Alifahamisha kwamba madhumuni ya kufanya  hivyo ni kutoa nafasi kwa muombaji alieandikishwa kuwasilisha malalamiko ya kurekebisha taarifa zake,  kuomba jina lake liingizwe katika orodha iwapo aliandikishwa lakini hakuorodheshwa au kuweka pingamizi dhidi ya taarifa za muombaji mwengine aliekatika orodha.

Hata hivyo alisema kuwa kufanya hivyo kutawawezesha kujua kama taarifa zao zimo  katika orodha au kujua iwapo taaarifa zao zimenakiliwa kwa usahihi au kuweka pingamizi kwa wasio na sifa. 

Hivyo aliwaomba Wadau wa Uchaguzi na wananchi kwa ujumla kuwahamasisha vijana walioomba kuandikishwa kwenda kuangalia taarifa zao, kwani kufika kwao vituoni kuangalia taarifa kutawahakikishia nafasi ya kuwemo katika Daftari na kuwa Wapiga Kura. 

Akitoa taarifa ya Tathmini ya zoezi hilo Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ndugu.Thabit Idarous Faina alisema kuwa Tume ilitarajia kuandikisha Wapiga Kura Wapya 162,606.

Hata hivyo alisema pamoja na kuonekana idadi hiyo ni ndogo  lakini wamefikia malengo yao ukilinganisha na Uandikishaji wa miaka uliopita.

Akitoa Tathmini ya Uandiskishaji kiwilaya Faina alisema kuwa Wilaya ambayo imeandikisha watu kidogo ni Mkoani iliyoandikisha watu 2,562 sawa na asilimia 21.41 ambapo walitarajia kuandikisha Wapiga Kura Wapya 11,964 ikifuatiwa na Wilaya ya Micheweni iliyoandikisha watu 2,628 kati ya 10,907 sawa asilimia 24.09 ya waliokuwepo katika matarajio ya kuandikishwa. 

Wilaya nyengine ni Wilaya ya Magharibi ‘A’ walioandikishwa ni 7,157 kati ya 28,677 sawa na asilimia 24.96  huku Wilaya ya Kusini imefikisha asilimia 60 kwa kuandikisha watu 2,875 kati ya 4,792 , Wilaya ya Kaskazini ‘A’ imeandikisha watu 7,265 kati ya watu 13,169 sawa na asilimia 55.17 na Wilaya ya Mjini imeandikisha watu 10,722 kati ya watu 19,272 sawa na asilimia 55.64%

Kwa upande wake Mkuu wa Kurugenzi ya Huduma za Uchaguzi Khamis Issa Khamis akizungumzia kuhusu zoezi la uwekaji wazi orodha ya Wapiga Kura na walioomba kuhamisha taarifa zao alisema, hadi kufikia Febuari 14, mwaka huu, jumla ya Wapiga Kura 302 wamewasilisha maombi ya kuhamisha taarifa zao kutoka eneo moja kwenda jengine la Uchaguzi. 

Hata hivyo alisema kuwa uhamisho wa taarifa za Wapiga Kura ni endelevu na kazi ya kupokea taarifa za wanaoomba kuhamisha inaendelea kufanyika katika Ofisi za uchaguzi za Wilaya kila siku kwa saa za kazi. 

Nao washiriki wa Mkutano huo wakiwemo viongozi wa vyama vya Siasa waliishukuru Tume kwa kuwashirikisha katika kila eneo la zoezi hilo ikiwemo upatikanaji wa  mawakala lakini changamoto ambayo wameipata ni kukosa fursa ya kushuhudia zoezi hilo. 

Hivyo waliiomba Tume hiyo kwa zoezi la Uandikishaji la awamu ya pili wapatiwe nafasi hiyo, suala ambalo lilitolewa ufafanuzi na Mkurugenzi wa Uchaguzi Thabit Idarusi Faina ya kuwa haliwezekani, kutokana Sheria ya Tume ya Uchaguzi haijaruhusu mwanasiasa kuingia katika vyumba vya Uandikishaji na badala yake kuwaweka mawakala wao.

 

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii