Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imewataka Wadau wa Uchaguzi katika Wilaya ya Chake Chake Pemba kuona kuwa zoezi la uendelezaji wa Daftari la kudumu la Wapiga Kura linalotarajiwa kuanza tarehe 9 mpaka 11 mwezi huu katika Wilaya hiyo ni haki yao ya msingi.

 

Hayo yalielezwa na Mkurugenzi wa Elimu ya Wapiga Kura na Mawasiliano ya Umma ZEC ,Juma Sanifu Sheha wakati akifunguwa Mkutano wa Wadau wa Uchaguzi wa Wilaya ya Chake chake wakiwemo viongozi wa Serikali,Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Vyama vya Siasa na Asasi za kiraia uliofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari Madungu Chake Chake Pemba.

Aliwataka Wadau hao kuzingatia suala la kudumisha amani na utulivu uliopo katika nchi ili zoezi hilo liweze kwenda vyema sambamba na kuwahamasisha wananchi wenye sifa kushiriki katika zoezi hilo.

Alieleza kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inawaomba wadau hao kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa wananchi wote wa Zanzibar kujitokeza ili kujiweka tayari  katika kushiriki kwenye Uchaguzi ujao wa mwaka 2025.

"Tunawaomba wananchi wote kila mwenye sifa za kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu afike kituoni na ahakikisha hakosi haki yake hiyo", alisema.

Alifahamisha kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar,itaendelea kuwashirikisha Wadau wake wa Uchaguzi hatua kwa hatua ili kuhakikisha inatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Sheria zilizowekwa.

Alisema Uandikishaji Wapiga Kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa awamu ya kwanza utaanza tarehe 9 mpaka 11 mwezi huu katika vituo vyote vilivyomo ndani ya Wilaya hiyo.Alieleza ili mwananchi ambae ana sifa ya Ukaazi, umri wa miaka 18 pamoja na kitambulisho cha Mzanzibar Mkaazi watahakikisha anaandikishwa kwenye Daftari hilo.

Kwa upande wake mshiriki wa Mkutano huo wa Wadau kutoka chama cha ACT,Maalim Saleh Nassor Juma aliishukuru Tume hiyo kwa hatua ya Uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linalotarajiwa kuanza katika Wilaya ya Chake Chake Pemba tarehe 9 mpaka 11 mwezi huu.

Alisema pamoja na maelezo mazuri waliyopatiwa lakini aliiomba Tume kutenda haki katika kufanikisha zoezi hilo linaloendana na Uchaguzi.

Nae Moh'd Haji Kombo kutoka Chama cha CUF , aliiomba Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC kurekebisha baadhi ya changamoto ndogo ndogo ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kama lilivyopangwa.

Hata hivyo alisema iwapo baadhi ya changamoto hizo zitafanyiwa marekebisho kabla itaondosha uhasama na Masheha wao ambao ni Mawakala wa Tume kwa mujibu wa Sheria.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii