Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) inatarajia kuanza zoezi la Uandikishaji Wapiga Kura Wapya 115,348 kwa upande wa Unguja Disemba 23 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mhe.Jaji Aziza Iddi Suwedi wakati akifungua mkutano wa wadau wa makundi maalum kuhusu zoezi la Uandikishaji Wapiga Kura Wapya katika ukumbi wa ZURA Maisara,Mjini Unguja.
Alisema hatua hiyo inafuata baada ya kumalizika kwa zoezi la Uandikishaji Wapiga Kura Wapya katika kisiwa cha Pemba ulioanza rasmi Disemba 2 na kumalizika Disemba 15 mwaka huu ambalo lilianza katika Wilaya Micheweni na kumalizika katika Wilaya ya Mkoani.
Alibainisha kwamba kwa Unguja zoezi hilo litaanza katika wilaya ya Kaskazini 'A' na kumalizika wilaya ya Mjini Januari 15 mwaka 2024.
Alisema kwa Kaskazini 'A' ZEC inatarajia kuandikisha Wapiga kura Wapya 13,169, Kaskazini 'B' Wapiga Kura 7,880, Kati Wapiga Kura 10,438, Kusini Wapiga Kura Wapya 4,792, Magharibi 'A' Wapiga Kura 28,677, Magharibi 'B' Wapiga Kura 31, 120 na wilaya ya Mjini Wapiga Kura wapya 19,272.
Makamu Aziza alisema ZEC kwa Uandikishaji huu inakadiria kuandikisha wapiga kura wapya wapatao 162,606 kutokana na makadirio ya takwimu ya Sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2022 kwa Unguja na Pemba.
Alibainisha kwamba Uandikishaji huo ni matayarisho ya Uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwani Uandikishaji huo ni wa awamu ya kwanza na awamu ya pili utafanyika mwanzoni mwa Uchaguzi mwaka 2025.
Akizungumzia lengo la kufanya mkutano huo alisem ZEC ina utaratibu wa kukutana na wadau kila linapotokea jambo muhimu ambalo linahitaji kushirikisha wadau.
Alisema madhumuni ya mkutano huo ni kutoa taarifa kwa wananchi kuhusiana na jukumu linaloikabili Tume na kuomba ushirikiano wao katika kufanikisha jambo hilo.
Alisisitiza kwamba Uandikishaji huo utawahusu wapiga kura wapya ambao hawajaandikishwa katika Daftari la Wapiga Kura ambapo zoezi litafanyika kwa muda wa siku tatu kwa kila kituo kilichowekwa na Tume hiyo.
Aliwaomba wananchi waliotimiza sifa kujitokeza kutumia haki yao ili waweze kushiriki katika Uchaguzi wa mwaka 2025.
Hivyo aliwasisitiza watu wote wenye sifa kujitokeza katika Uandikishaji huo hasa Makundi ya Watu wenye Mahitaji Maalum ikiwemo watu Wenye Ulemavu kwani makundi hayo yanapaswa kuzingatiwa na kupewa kipaumbele katika Uandikishaji na hata katika Uchaguzi kwani kufanya hivyo ni kuitendea haki Sera ya Jinsia na ushirikishwaji wa Makundi Maalum ya mwaka 2015 ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC.
Aliwaomba wananchi na wadau wote wa Uchaguzi wa Zanzibar kudumisha Amani katika kipindi chote cha Uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya kama walivyofanikisha katika kisiwa cha Pemba na matumaini yake kwamba wataendelea kushirikiana katika mustakabali mwema wa Uchaguzi wa taifa.
Nae Yumna Mmanga Omar kutoka Chama cha Maalbino, Bakar Omar Hamad kutoka Jumuiya ya JUWAUZA na Abdalla Alawi Abdalla kutoka Chama cha Viziwi Zanzibar, waliiomba ZEC kuweka takwimu za watu Wenye Ulemavu ambazo zitasaidia kupata vifaa vya watu hao ikiwemo karatasi za nukta nundu kwa wasioona.
Waliomba ZEC kuelimisha makarani kutumia lugha nzuri kwa wapiga kura ikiwemo watu wa Makundi Maalum.
"Ni lazima makarani wapewe Elimu hasa wanapokwenda watu Wenye Ulemavu wa aina zote kwani watu hao wanakuwa wakali na watu hao wanaohitaji huduma kama watu wengine katika uandikishaji huo,"
Mbali na hayo walioshauri tuke Uchaguzi kukaa na vyama siasa kuendesha kampeni za kistaarabu kwa kunadi sera na sio kutoa kauli ambazo zinaviashiria vya uvunjifu wa amani kwani viashiria hivyo vitasababisha kundi hilo kutojitokeza katika upigaji wa kura na kukosa haki yao ya msingi kikatiba.
Walishauri jumuiya zilizoshiriki kuhakikisha wanawafikia wenzao ili kuona idadi ya watu Wenye Ulemavu inaongezeka katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mwaka huu.
Katika mkutano huo mada mbili zilijadiliwa ikiwemo ya taarifa na utaratibu wa Uandikishaji wa Wapiga Kura na Uendeshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na nafasi ya sheria ya Uchaguzi katika Uandikishaji na Uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,Mkutano huo umeshirikisha makundi mbalimbali ikiwemo Chama cha Viziwi Zanzibar, Chama cha Wasiiona, Chama cha Maalbino Jumuiya ya Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, mabaraza ya vijana na makundi ya wanawake.