Na Ahmed A. Mohammed= ZEC

 

Tume ya Uchaguzi ya Serikali ya Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Aboud Jumbe Mwinyi  imepatiwa Elimu ya Wapiga Kura na Tume ya  Uchaguzi ya Zanzibar  ili kupata uelewa wa uendeshaji wa Uchaguzi Skulini hapo.



Elimu hiyo imekuja kufuatia maombi maalum yaliyoombwa na Uongozi wa Skuli hiyo chini ya Mwalimu Mkuu  Bi.Mwanamzaka Muazini Bakari kwa lengo la kuongeza uelewa kwa Tume hiyo kuelekea katika Uchaguzi wa Serikali ya Wanafunzi kwa mwaka 2024/2025.

Akizungumza na  Wanafunzi hao ambao walichaguliwa na Uongozi wa Skuli hiyo kusimamia zoezi hilo la Uchaguzi Skulini hapo, Mkuu wa Kurugenzi ya Elimu ya Wapiga Kura na Mawasiliano kwa Umma ndugu. Juma Sanifu Sheha  amewataka wanafunzi hao kuitumia Elimu hiyo ili kufanya Uchaguzi  huru na haki sambamba na kuifanyia kazi kwa maslahi ya baadae watakapomaliza masomo yao na kuwa uraiani.

"Tunaelewa hapa kati yenu wapo ambao ni miongoni mwa Wapiga Kura na munajua taratibu za Kupiga Kura na  wapo watakaokuwa Wapiga Kura, Viongozi  na wasimamizi  watarajiwa katika Uchaguzi hivyo elimu hii ikawe muongozo wenu juu ya namna ya Kupiga Kura kwa kufuata  Sheria na taratibu ”  alisema.

"Elimu hii tuliyowapa  kuelekea Uchaguzi wenu  wa   kuwapata viongozi wa Serikali ya Wanafunzi  haina tofauti na Elimu ya Wapiga Kura katika Uchaguzi Mkuu wa Kitaifa hivyo  ni matumaini yangu mtaitumia leo mkiwa hapana hapo mkitoka   kwenda katika jamii itakapohitajika muda wenu utakapofika wa kushiriki Uchaguzi  Mkuu wa Kitaifa" alisema.

akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi la Utoaji wa Elimu ya Wapiga Kura kwa Tume hiyo ya Uchaguzi ya Serikali ya Wanafunzi Skuli hapo, Bi Ilham Mukhlis Othman ambae ni Mwalimu na Katibu wa Serikali ya Wanafunzi Skuli ya Aboud Jumbe Mwinyi ameishukuru Tume hiyo kwa kuwapatia Elimu itayowasaidia kurahisisha zoezi la Uchaguzi na kuwa Uchaguzi wa huru,haki na Salama.

Sambamba na hilo ametoa wito kwa Skuli nyengine  kuomba kupatiwa Elimu hiyo kutoka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kabla ya kufanya Uchaguzi wa Serikali ya Wanafunzi Maskulini kwao

"Wito wangu kwa Skuli nyengine kabla ya kufanya Uchaguzi lazima tupate wakufunzi husika wa Uchaguzi ili vijana wapate Elimu na kama tunavyojua vijana wetu bado ni wadogo na hawajawahi Kupiga Kura za Kitaifa Kura zao ni za Skuli tu, kwaiyo ni lazima kwanza wapewe Elimu ya Wapiga Kura kwani Elimu hiyo wataitumia hapa Skuli na katika Jamii kwa Ujumla” alisema.

Nao Wanafunzi waliopewa Elimu hiyo wameishukuru na kuipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa Elimu hiyo kwani wamejifunza vitu vingi ambavyo walikuwa hawavifahamu.

Zoezi la Uchaguzi Skulini hapo limefanyika tarehe 03 Septemba 2024 ambapo wanafunzi walichagua Rais na Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi Skulini hapo.

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii