Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, amewataka wakandarasi waliopewa ujenzi wa miradi ya maendeleo hapa nchini kuhakikisha wanaheshimu mikataba ya makubaliano.

Mhe.Hemed Suleiman Abdulla  alieleza hayo jana wakati alipofanya  ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Afisi Kuu ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) iliyopo Maisara mjini Zanzibar.

Alisema kumekuwa na  tabia inayoanza kuzoeleka kwa baadhi ya wakandarasi kuchelewesha miradi kwa wakati, jambo ambalo linakwamisha azma ya Serikali ya kutatua kero za wananchi

Alisema kuwa, Serikali itaendelea kuheshimu mikataba inayoingia na kampuni mbalimbali na kutoa ushirikiano kwa kampuni zinazojenga miradi ya maendeleo nchini ili kuharakisha ukamilishaji wa miradi hiyo kwa wakati.

Makamu wa Pili wa Rais, alisema kumalizika kwa wakati kwa ujenzi wa jengo hilo kutatoa fursa kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kutekeleza majukumu yake kwenye mazingira mazuri na salama kulingana na umuhimu wa Afisi hiyo

Sambamba na hayo, alisema kuanzia sasa, Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA) wanapaswa kuchukua hatua stahiki dhidi ya kampuni ambazo hazitokabidhi miradi kwa wakati uliopangwa ili iwe fundisho kwa kampuni nyengine.

Aidha,aliwataka Wakala wa Majengo kuacha muhali kwa kampuni yoyote itakayo kwenda kinyume na mkataba wa ujenzi wa miradi ya Serikali ambayo imefungwa baina ya Serikali na kampuni husika.

Nae ,mkandarasi kutoka kampuni ya China Railway Jianhuwang Engineering (CRJE), Chey Yur, alisema licha yakukabiliwa na changamoto mwanzoni mwa ujenzi huo, lakini watahakikisha wanakamilisha na kukabidhi jengo hilo ndani ya muda waliokubaliana

Mkandarasi huyo, alisema wameshaongeza nguvu kazi katika ujenzi huo na wanatarajia kuanza kufanya kazi mchana na usiku ili kuongeza kasi ya ujenzi na kukamilisha kwa wakati uliopangwa na kwa ubora zaidi.

Kwa upande wake, msimamizi wa majengo kutoka ZBA Mohamed Nahoda Mohamed, alisema ZBA wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na mkandarasi wa ujenzi huo ambao kwasasa umefikia asilimia 20 ya ujenzi na wanatarajia kukamilisha mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu.

Ujenzi huo, wa jengo la ghorofa nne la Afisi kuu ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, utakapokamilika utagharimu zaidi ya bilioni 11 ambazo utajumuisha Afisi , kumbi za Mikutano na vyumba kwa ajili ya wageni.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii