Wapiga Kura Wapya 44,595 wamepatiwa vitambulisho vya Kupigia Kura Unguja na Pemba kwa zoezi la Uandikishaji Wapiga Kura Wapya.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Ndugu.Thabit Idarous Faina wakati akizungumza na Waandishi wa habari huko Ofisini kwake Maisara,Mjini Unguja.
Mkurugenzi Faina alisema, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar iliandikisha jumla ya wananchi 57,883 kwa Unguja na Pemba kwa mwaka wa 2023/2024 ambapo zoezi hilo lilifuatiwa na Display (Uwekaji wazi wa Orodha ya Wapiga Kura) na hakukuwa na mwananchi aliyepigwa katika zoezi hilo au kukataliwa kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Akielezea baadhi ya mafanikio ya zoezi hilo amesema,wananchi wamekuwa na muamko mkubwa wa kuitikia wito wa zoezi hilo na kupenda kuifahamu michakato ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar jambo ambalo limekuwa likitoa mashirikiano mazuri baina ya Tume na wananchi hao.
“Tume katika kutekeleza majukumu yake wananchi wamekuwa wa kwanza kuuliza hasa wanapokosa fursa kwa mambo wasiyoyajua” alisema.
Ndugu Faina aliendelea kusema kuwa, Takriban ya asilimia 77% ya vitambulisho hivyo vimechukuliwa na wananchi wenyewe,aliongeza kuwa, zoezi hili halimgharimu kitu chochote mwananchi zaidi ya risiti yake au kitambulisho chake cha Mzanzibari Mkaazi chenye utambulisho wa taarifa zake.
Katika mazungumzo yake, Mkurugenzi alisisitiza kuwa, Tume itahakikisha kila mwananchi aliyejiandikisha anapata kitambulisho chake cha Kupigia Kura pamoja na kukamilika ratiba ya siku mbili za Jumamosi na Jumapili kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya utoaji wa vitambulisho katika vituo vilivyotumika kwa zoezi hilo Unguja na Pemba, aidha, aliwaomba Wapiga Kura Wapya waliojiandikisha ambao hawajachukua vitambulisho vyao,kuendelea kujitokeza katika Afisi za Uchaguzi za Wilaya kwani zoezi hilo ni endelevu hadi ifikapo mwaka 2025 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Akizungumzia changamoto zilizojitokeza katika zoezi hilo Mkurugenzi Faina alisema,wapo baadhi ya wananchi ambao hawakutoa taarifa sahihi hasa nambari zao za simu, hivyo amewaasa wananchi kuweka taarifa zao sahihi ili kurahisisha kuwapatia taarifa zao hasa pale wanapohitajika kwa haraka.
Mkurugenzi Faina aliwaomba waandishi wa habari kuendelea kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar pamoja na kuwaelimisha wananchi juu ya matumizi ya huduma ya Simu ya mkononi ambapo mwananchi anaweza kupata taarifa zake za Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kupiga nambari *152*00# huduma hii ni bure kwa mitandao yote iliyosajiliwa nchini Tanzania.
Zoezi la Uchukuaji wa vitambulisho vya kupiga kura lilianza tarehe 25 Mei 2024 na kukamilika tarehe 23 Juni mwaka huu katika Shehia 407 za Wilaya zote za Unguja na Pemba ambapo pia zoezi kama hilo la Uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya litafanyika tena mwanzoni mwa mwaka 2025.