Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imetoa wito wa kuvumiliana miongoni mwa wanafunzi katika Uchaguzi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Tawi la Zanzibar (Karume Campus Zanzibar).

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Divisheni ya Utunzaji Kumbukumbu Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Othman Maulid Vuai wakati akiwasilisha mada ya uvumilivu wa kuyapokea matokeo katika mafunzo ya Elimu ya Wapiga Kura kwa Wagombea wa Urais,Mawakala wa Wagombea,Wagombea wa nafasi mbali mbali katika ngazi za Chuo, Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho.

Alisema lengo la utolewaji wa mada hiyo kwa wanafunzi ni kuhimiza utulivu, uvumilivu na mshikamano kabla na baada ya matokeo ya Uchaguzi kutangazwa  ili kudumisha amani na umoja uliopo Chuoni hapo, kwani Uchaguzi una matokeo mawili ya kushinda au kushindwa hivyo si vyema kuleta migawanyiko baina ya Wanafunzi ambayo inaweza kuhatarisha usalama na kuleta chuki baina yao.

 

Amewaasa  kushiriki katika mchakato wa Uchaguzi kwa salama na amani na yule atakaeshindwa katika Uchaguzi asikate tamaa kwani anaweza kuomba nafasi kushiriki tena katika Chaguzi zijazo.

Na kwa Upande wake Khamis Ali Juma ambae ni mwanafunzi na Mgombea wa Urais katika Uchaguzi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere aliahidi kwa niaba ya washiriki wenzake kuyafanyia kazi na kuyapokea mafunzo hayo hasa suala hili la kuyapokea na kuyakubali matokeo kwani lina umuhimu mkubwa katika Uchaguzi huo.

 

Amewaomba wanafunzi wenzake kujitokeza kwa wingi katika Uchaguzi ili kuchagua kiongozi atakaewawakilisha katika kutetea maslahi ya wanafunzi kwa Uongozi pamoja na kuwawakilisha ndani na nje ya nchi.

Akitoa ufafanuzi juu ya maswali mbali mbali yaliyoulizwa wakati wa utolewaji wa Elimu ya Wapiga Kura,Mkuu wa Kurugenzi ya Elimu ya Wapiga Kura na Mawasiliano kwa Umma ndugu.Juma Sanifu Sheha alisema,Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imekuwa ikitoa Elimu ya Wapiga Kura kwa Taasisi mbali mbali za elimu ili kuhakikisha Uchaguzi unakuwa huru na wa haki lakini pia kupunguza idadi ya Kura kuharibika.

Uchaguzi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Tawi la Zanzibar utafanyika siku ya Ijumaa ya tarehe 17 Mei 2024 ambapo wanafunzi Chuoni hapo watachagua viongozi mbali mbali ikiwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuoni humo.

 

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii