Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera Uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe.Hamza Hassan Juma ameishauri Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kuendeleza mashirikiano katika Ujenzi wa Mradi Afisi Mpya za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.
Waziri ameyasema hayo wakati wa ziara ya kikazi alipotembelea Mradi wa wa Ujenzi wa Afisi Kuu ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Maisara,Mjini Unguja.
Amesema lengo la kutembelea Mradi huo ni kutambua hatua uliyofikia ili zitakapofika Sherehe za Mapinduzi mwakani, Serikali itambue ni Miradi mingapi inatarajia kuweka mawe ya msingi na kuizindua.
Ameipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa maendeleo ya Mradi huo na kuhimiza kuendeleza mashirikiano na kujipanga vizuri kuwasimamia wakandarasi kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuepusha kujitokeza kasoro katika ujenzi huo.
Ametoa rai ya kufanya vikao vya mara kwa mara (site meetings) ili kuepusha mkwamo baina ya Serikali na Mkandarasi wa Mradi huo ili kuona kila kitu kinakwenda vizuri na Serikali itajitahidi kuendelea kuzitatua changamoto ikiwemo kucheleweshwa kwa malipo kwa Mkandarasi ili kazi hiyo iendelee vizuri.
Nae Mkurugenzi wa Uchaguzi ndugu.Thabit Idarous Faina ameishukuru Kampuni ya CRJE inayojenga Mradi huo pamoja na Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA) kwa mashirikiano mazuri kwani wamekuwa wakifanya vikao vya mara kwa mara na matarajio ya ujenzi wa Mradi huo ni mazuri sambamba na hilo ameishukuru Serikali kwa kuhakikisha upatikanaji wa fedha inayohitajika katika Mradi huo.
Na kwa upande wa Wakandarasi wa Mradi huo wameahidi kufikia malengo yaliyowekwa ya kuhakikisha Mradi huo unakamilika kama muda ulivyopangwa kwa mwaka huu.