Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imewataka wanafunzi wa elimu ya ngazi ya juu kujitokeza kwa wingi katika zoezi la Uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya ili kuendeleza demokrasia nchini.
Yamesemwa hayo na Mkuu wa Kurugenzi ya Elimu ya Wapiga Kura na Mawasiliano ya Umma ndugu.Juma Sanifu Sheha wakati wa utoaji wa elimu ya Wapiga Kura kwa wanafunzi wa Chuo cha Utawala wa Umma (The Institute of Public Administration) kilichopo Tunguu, Mkoa wa kusini Unguja.
Alisema Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inatarajia kuanza zoezi la Uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya kwa awamu ya kwanza kuanzia Disemba 2 mwaka huu ambapo zoezi hilo litaanzia katika Wilaya ya Micheweni na kumalizika tarehe 15 Januari 2024 katika Wilaya ya Mjini hivyo ni wajibu wa kila mwanafunzi mwenye sifa za kuandikishwa ajitokeze katika zoezi hilo na kwa kufanya hivyo ni kuendeleza demokrasia nchini.
Wakati akiyasema hayo aliongeza kuwa,Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imekuwa ikitoa taarifa mbalimbali katika Vyombo mbalimbali vya Habari na mitandao ya kijamii kuhusu zoezi la Uandikishaji hivyo ni vyema kufuatilia vyanzo sahihi ili kupata taarifa sahihi juu ya zoezi hilo.
Nae Salim S. Salim ambae ni mwanafunzi wa Shahada ya kwanza ya Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia ambae pia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar (The Institute of Public Administration) aliishukuru Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kuwapatia mafunzo ya elimu ya Mpiga Kura lakini pia ameahidi kuwashajihisha wanafunzi wengine wayafanyie kazi mafunzo hayo na wameahidi kujitokeza kwa wingi kwa kila ambae hajajiandikisha atajiandikisha katika awamu hii.
Kwa upande mwengine,nae Nadhra A. Mussa ambae ni mwanafunzi wa Shahada ya kwanza ya Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia ambae pia ni mwanafunzi na mgombea Urais wa Serikali ya wanafunzi alisema,Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imefanya jambo zuri kuwapatia elimu hiyo kwani hawakuwa na uelewa wa kutosha juu ya masuala mengi yanayohusu uendeshaji wa zoezi la Uchaguzi na kwa elimu hiyo watafanyia kazi kila walichoelekezwa ikiwemo kujitokeza katika zoezi la Uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya.
Mafunzo hayo ya siku moja ya Elimu ya Mpiga kura yametolewa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali ya Wanafunzi unaotarajia kufanyika siku ya Ijumaa ya tarehe 24 Novemba 2023.