Mweyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Mhe.Jaji George Joseph Kazi  amewataka wafanyakazi kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya kisheria, kuongeza ushirikiano na kufanya kazi kwa bidii ili kuimarisha utendaji kazi wa Tume hiyo.

Mwenyekiti Ameyasema hayo leo wakati alipokutana na wafanyakazi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa Afisi zote za Unguja na Pemba kwa lengo la kuwatambua wafanyakazi wake pamoja na kujadili masuala mbali mbali ikiwemo changamoto zinazowakabili wafanyakazi katika utendaji wao wa majukumu yao ya kazi ya kila siku.

Amesema ili Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar iyafikie malengo yake yanayotarajiwa ni wajibu wa wafanyakazi kufuata Sheria za utumishi, kudumisha mashirikiano na kufanya kazi kwa bidii kwani Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ni moyo wa visiwa vya Zanzibar katika suala zima la kudumisha amani na kwa kiwango kikubwa ni chanzo cha maendeleo nchini.

Amesema, kwa upande wa utendaji kazi anapenda kuona maendeleo mazuri katika ufanyaji wa kazi na hatovumilia uzembe wa aina yeyote utakaofanyika katika utekelezaji wa majukumu kwa wafanyakazi wa Tume hiyo.

Aidha amefahamisha kuwa katika ufanyaji kazi wa wafanyakazi ni vyema kuzingatia Sheria za utumishi kwani ndio muongozo juu ya namna ya utendaji kazi wa kila siku.

Wakati akiyaeleza hayo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar amesema Taasisi mbalimbali zinakabiliwa na changamoto za ukosefu wa nidhamu ya   Wafanyakazi ikiwemo utoro na uchelewaji kazini,uzembe katika Uwajibikaji, uchafu katika mazingira ya kazi  hivyo si vyema kwa watumishi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kuwa na tabia hizo ili kuijengea picha nzuri Afisi hiyo na pia amewahakikishia kuwa  mstari wa mbele katika kusimamia maendeleo ya wafanyakazi wa Tume hiyo.

Akifugua mjadala katika Mkutano huo ndugu.Saadun Ahmed ambae ni Mkuu wa Kurugenzi ya Utawala, Mipango na Rasimali watu amempongeza Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kuitisha kikao hicho kwani ni ishara njema katika kujenga uhusiano mzuri baina ya Tume na Wafanyakazi wake.

Amesema wafanyakazi wa Tume hiyo wakiwemo Wakuu wa Kurugenzi,  Wasimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ,Wakuu wa Divisheni na Maafisa wa Tume watahakikisha maelekezo yaliyotolewa na Mwenyekiti kuwa ni yenye kuzingatiwa na yanafanyiwa kazi na yeyote atakaekiuka misingi ya kazi hatua za kinidhamu zitachukuliwa. 

Akichangia Mjadala katika kikao hicho ndugu.Juma Sanifu Sheha ambae ni Mkuu wa Kurugenzi ya Elimu ya Mpiga Kura na Mawasiliano Kwa Umma amemueleza Mwenyekiti kuwa, nguvu kubwa ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ni utendaji kazi kwa mashirikiano ila licha ya kuwepo kwa jambo hilo bado Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa wafanyakazi kwa baadhi ya divisheni  hivyo ni vyema Tume ya Uchaguzi ikalitazama hilo kwa jicho la makini ili kuongeza kasi ya utendaji kwa Tume hiyo.

Akifunga Mkutano huo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ameahidi kufanya kazi kwa pamoja na Wafanyakazi wa ngazi zote wa Tume ya hiyo na yeye ni mtu anayefikika hivyo ni vyema kutosita kushirikiana nae kwa mambo ya ndani ya Tume na nje ya Tume hasa masuala ya kijamii ili kujenga mahusiano mazuri baina yake na watendaji wake.

  

 

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii