NA AHMED A. MOHAMMED-ZEC

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imeahidi kuendelea na zoezi la utoaji wa elimu ya Mpiga kura ili kuhakikisha Taasisi za Elimu visiwani Zanzibar zinakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya uchaguzi kwa wanafunzi na watumishi wa Taasisi hizo.

Hayo yamesemwa na Afisa Elimu ya Wapiga Kura Ndugu.Said Ramadhani Mgeni wakati akitoa  mafunzo ya Elimu ya Wapiga Kura kwa Wanafunzi wa skuli ya Sekondari ya Glorious Academy iliyopo Mpendae,Wilaya ya Mjini Unguja,ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali ya Wanafunzi kwa skuli hiyo,Uchaguzi ambao utafanyika siku ya Ijumaa ya tarehe 25/08/2023 saa 2:00 za asubuhi.

Akifungua Mafunzo hayo Ndugu.Said Ramadhani Mgeni aliwaeleza Wanafunzi na Walimu wa Skuli hiyo,Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inajukumu la utoaji wa Elimu ya Wapiga Kura ili kuhakikisha Wananchi wote visiwani Zanzibar wanakuwa na uwelewa wa kutosha katika masuala ya Uchaguzi,hivyo wataendelea kutoa Elimu ya Mpiga kura kila inapohitajika kwa Taasisi yoyote ya Serikali au Taasisi Binafsi.

Akiendelea na mafunzo hayo,Afisa  Elimu Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa Wanafunzi na Walimu hao alisema,ili uweze kuwa na sifa za kuandikishwa kuwa Mpiga kura au Kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi  ni lazima uwe na sifa ambazo zimewekwa kisheria,na kwa upande wa sifa za kuandishwa kuwa Mpiga Kura, miongoni mwao Mtu kuwa na umri usiopungua miaka 18,awe na kitambulisho cha Mzanzibar Mkaazi,awe ni Mkaazi wa kudumu wa eneo husika si chini ya miezi 36 mfululizo na sifa hizo zimeelezwa katika kifungu namba 12.-(1) na kwa nafasi ya Urais miongoni mwa sifa za kugombea  ni kuwa Mzanzibar wa kuzaliwa au Kuwa na umri usiopungua miaka 40 kama ilivyoelezwa katika Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2018 kifungu namba 43,na kwa nafasi ya Uwakilishi na Udiwani miongoni mwa sifa za kugombea  awe Mzanzibari na awe na umri usiopungua miaka 21 kama ilivyoelezwa katika Sheria hiyohiyo ya Uchaguzi Kifungu namba 44 na 45.

Sambamba na hayo Ndugu.Said Ramadhani Mgeni aliwaeleza Wanafunzi na Walimu hao alama zinazokubalika na zisizo kubalika katika karatasi ya Kura na utaratibu wa Uchaguzi unavyofanyika ambapo Wapiga Kura hupaswa kukaa kwa mstari kwa kuzingatia jinsia lakini pia kuwapa kipaumbele watu wenye mahitaji maalumu ikiwemo Watu Wenye Ulemavu,Wajawazito na wenye Watoto Wachanga na Wazee wasiojiweza,

Katika Mafunzo hayo Afisa Elimu Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar aliambatana na Afisa Mipango Saada Ubwa Hassan,ambae aliwapatia elimu juu ya nani wanaoruhusiwa kuwa ndani ya vituo vya Kupiga kura na kuhesabu kura na Afisa  Tathmini na Ufuatiliaji Juma Suleiman Juma,ambae nae alieleza makosa ya Kiuchaguzi sambamba na kuwapa Nafasi Walimu na Wanafunzi wa shule hiyo kuuliza maswali mbalimbali ili yapate kutolewa ufafanuzi.

Nae,Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Glorious Academy Bi.Rukia Ali Omar ameipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwani Wanafunzi hao wapo ambao wameshafikia umri wa kupiga Kura hivyo Elimu hiyo ni muhimu sana kwa Wanafunzi hao ili waweze kupata uelewa kwani hii ni moja ya haki yao ya msingi, ameziomba Taasisi nyengine za Kielimu zisisite kufika Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ili kuomba kupatiwa vifaa na mafunzo ya Kupiga Kura kila wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Wanafunzi unapofanyika.

Nae,Sahim Juma Salim Mwanafunzi wa kidato cha sita shuleni hapo ambae pia ni Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Skuli  ya Glorious Academy ambae anamaliza muda wake ameishukuru Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufika Skulini hapo na kutoa mafunzo hayo wameahidi kuyapokea ili kwa wale ambao wameshatimiza umri waweze kuitumia haki yao muda ukifika.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar katika mafunzo hayo imewapa elimu ya Wapiga Kura jumla ya Wanafunzi 472  na Walimu 19 ambao kwa pamoja wameishukuru Tume kwa kufika shuleni hapo. 

 

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii