NA AHMED A. MOHAMMED-ZEC
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imetoa mafunzo ya nadharia na vitendo kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari ya DKT.Salim Ahmad Salim kwa lengo la kuwajengea uelewa juu ya zoezi zima la Uchaguzi unavyofanyika.
Mafunzo hayo yametolewa na Maafisa kutoka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Kisiwani Pemba siku ya Alhamis ya tarehe 17/08/2023 katika skuli hiyo iliyopo Chakechake Shehia ya Wara Kisiwani Pemba,ambapo wanafunzi 641 na walimu wa skuli hiyo walishiriki mafunzo hayo,ikiwa pia ni maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali ya Wanafunzi wa Skuli hiyo,Uchaguzi ambao ulifanyika siku ya Ijumaa ya Tarehe 18/08/2023 majira ya saa 3:30 za Asubuhi.
Akifungua mafunzo hayo Afisa Uchaguzi Wilaya ya Chakechake Ndugu.Abdallah Juma Abdallah na Ndugu.Juma Mkubwa Issa ambae ni Afisa elimu ya Wapiga Kura Pemba amesema lengo la mafunzo hayo kwa wanafunzi ni kuwapatia uelewa ili wapate kuyatambua majukumu mbali mbali ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na namna ya Uchaguzi unavyoendeshwa, elimu ambayo itawawezesha kushiriki vyema katika ujenzi wa utawala bora.
Aidha,aliwaeleza wanafunzi hao elimu juu ya mwenendo mzima wa Uchaguzi na Kura ya Maoni inavyofanyika ili kuwasaidia wanafunzi kuelewa juu ya namna ya uteuzi wa Serikali unavyofanyika ikiwemo Serikali mbili,tatu au Serikali ya umoja wa kitaifa,kuanzia mchakato mzima wa maoni hadi siku ya Uchaguzi ambayo wananchi huchagua viongozi wanaowataka,
Nae ndugu. Juma Mkubwa ambae ni Afisa Elimu wa Tume hiyo Kisiwani Pemba licha ya kutoa elimu juu ya masuala mbali mbali ikiwemo zoezi zima la kugombea nafasi mbali mbali wakati wa Uchaguzi pia aliwapa wanafunzi hao nafasi ya kuuliza na kujibu maswali mbali mbali ili kupima uelewa wao wakati wa utoaji wa mafunzo kwa wanafunzi hao.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo ndugu.Khamis Said Othman aliwaasa Walimu na Wanafunzi ambao wameshiriki katika mafunzo hayo kuipokea elimu hiyo ya dhana nzima ya Uchaguzi kwani tukio hilo limebeba mazingatio makubwa kwa maisha yao ya sasa na baadae.
Nae Rais mstaafu wa Serikali ya Wanafunzi wa Shule hiyo Mustafa Kassim ameishukuru Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufika Shuleni kwao na kuwapatia mafunzo hayo kwani yatawasaidia katika kuzitambua haki zao na kuyatambua masuala mbalimbali ya kisiasa.
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imekuwa ikishirikiana na Taasisi mbali mbali Binafsi na za Serikali katika kuzipatia mafunzo ya Elimu ya Mpiga Kura.