Na Ahmed A. Mohammed = ZEC
Jeshi la Zimamoto na Uokozi Zanzibar limetoa mafunzo ya siku moja ya nadharia na vitendo ya elimu ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto kwa wafanyakazi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) katika Afisi kuu za Tume hiyo zilizopo Maisara mjini Unguja,
Nae Mkufunzi Mkuu wa mafunzo hayo, kutoka kitengo cha mafunzo Jeshi la Zimamoto na Uokozi Zanzibar ,S/SGT Muhidini Mzee Ame amesema kuwa, mara nyingi wananchi na watumishi wa taasisi mbalimbali binafsi na za kiserikali wamekuwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu kujiokoa pindi wanapopata matatizo ya moto, hivyo Jeshi hilo limelenga kuwapa ujuzi wa kujikinga na kupambana na ajali za moto ili kuepusha au kupunguza athari zinazoweza kutokea ikiwa janga hilo litatokea,aidha ni vyema elimu kama hizi zikazingatiwa na kufanyiwa majaribio mara kwa mara kwa jamii na taasisi mbalimbali,
Kwa upande wa Mkufunzi Msaidizi wa Zimamoto na Uokozi Zanzibar CPL.Mohammed Haji Vuai ambaye alikuwa mwezeshaji wa mafunzo hayo kivitendo aliwaeleza washiriki kuhusu mifumo mbalimbali mahususi kwa ajili ya kujikinga na kujiokoa dhidi ya majanga ya moto na alitaja baadhi ya mifumo ikiwemo vigunduzi moshi, vizima moto, alama za njia za dharura na eneo maarufu kama “Refugees Area” au kitaalamu likiitwa “Balcon” aidha, katika mafunzo hayo, washiriki walifundishwa namna ya kuukabili moto kwa kutumia vifaa vya kuzimia moto vilivyopo katika mazingira mbalimbali vikiwemo mchanga mkavu,matawi ya miti mibichi, mitungi ya gesi ya kuzima moto (fire extinguishers), Blanketi maalum (fire blanket) na mfumo wa maji ya kuzima moto kwa mpira (horse reel).
Kwa upande mwengine nae Mkuu wa Kurugenzi ya Mipango,Rasimali watu na Utawala ndugu.Saadun Ahmed Khamis ambae ni moja ya washiriki wa mafunzo hayo amelishukuru jeshi la Zimamoto na Uokozi Zanzibar kwa kuwapatia mafunzo hayo kwani mafunzo hayo yana faida mbalimbali ambazo zinawapa uelewa juu ya kupambana na majanga ya moto ikiwemo kuokoa mali za Serikali katika Afisi na maghala ya Serikali,wakati akiyasema hayo ameliomba jeshi la Zimamoto na Uokozi Zanzibar kuwapatia mafunzo hayo mara kwa mara ilikuzidi kuongeza uelewa juu ya kupambana na majanga ya moto na ameomba kuboresha mashirikiano na taasisi hiyo kwa kuwatembelea mara kwa mara,
Sambamba na hilo,ndugu Saadun Ahmed Khamis ametoa wito kwa taasisi binafsi na za kiserikali kuwapatia mafunzo watumishi wake kwani itaongeza tahadhari ya kujinga na majanga ya moto,
Mafunzo hayo yaliyotolewa na jeshi la Zimamoto na Uokozi kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ni utekelezaji wa mkakati wa kuimarisha usalama wa watumiaji wa jengo na mali za Afisi na pia ni takwa la kisheria kupitia Kanuni za Jeshi la Zimamoto na Uokozi Zanzibar za sheria namba 7 ya mwaka 1999 kuhusu kuwezeshwa kimafunzo juu ya tahadhari za kuchukuliwa na watumiaji wote wa jengo katika jitihada za kupambana na majanga ya moto.