Na Jaala Makame Haji - ZEC

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Jaji Mkuu (Mst) Mheshimiwa Hamid Mahmoud Hamid amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe maalum wa Maafisa kutoka umoja wa Mataifa (UN) Ofisini kwake Maisara Mjini Zanzibar.

Ujumbe wa Maafisa hao ukiongozwa na Afisa Mkuu wa Uchaguzi katika Idara ya Siasa na masuala ya Ujenzi wa Amani Akinyemi Adegbola ulifanya mazungumzo na Mwenyekiti Hamid kuhusiana na masuala ya tathimini ya demokrasia ya Uchaguzi nchini Tanzania ambapo ndugu Akinyemi kupitia Shirika la Kimataifa la Mipango ya Kimaendele UNDP ameuahidi uongozi wa Tume kuendelea kushrikiana nao katika uimarishaji wa Demokrasia kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

Katika mazungumzo hayo Mheshimiwa Hamid Mahmoud akiwa pamoja na Makamishina wa Tume alielezea kuridhishwa kwake kutembelewa na ujumbe huo ambapo aliahidi kuunga mkono nia na dhamira ya Umoja wa Mataifa ya kusimamia demokrasia ambayo wamekuwa wakiitekeleza kwa miaka mingi hasa katika kuisadia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar wakati wa kipindi cha Uchaguzi.

Ujumbe huo pia ulipata nafasi ya kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi Khamis Kona Khamis pamoja na watendaji wa Tume hiyo juu ya mustakabali na mwelekeo wa uimarishaji wa shughuli za Uchaguzi ujao mwaka 2025.

Awali ujumbe huo ulifanya mazungumzo na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemedi Suleiman Abdullah na baada ya mazungumzo na uongozi wa Tume na Watendaji wake walikukutana pia na Wadau wengine wa Uchaguzi akiwemo Kamishina wa Polisi Zanzibar, Naibu Msajili wa vyama vya siasa, Vyama vya Siasa na Asasi za Kiraia kwa lengo la kutoa maoni yao juu ya uimarishaji wa demokrasia kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Ndugu Akinyemi katika Ujumbe wake aliambatana na ndugu Mikyong Kim ambaye ni Afisa wa Masuala ya Siasa na Uchaguzi katika Divisheni ya Misaada ya Uchaguzi kutoka Umoja wa Mataifa, Ndugu Roselyn Akombe Mratibu wa Utawala bora na Ujenzi wa Amani kituo cha huduma za kikanda kwa Afrika (UNDP) na Bibi Vivianne Lugulu Afisa wa masuala ya siasa UNDP divisheni ya Afrika Mashariki.

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii