Na Jaala Makame Haji-ZEC
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe. Jaji Mkuu (Mst) HAMID MAHMOUD HAMID alisema Uteuzi wa wagombea wa kiti cha Urais unafanyika kwa mujibu wa maelekezo ya kifungu cha 26 cha Katiba ya Zanzibar, 1984 na kifungu cha 43 cha Sheria ya Uchaguzi Nam. 4 ya mwaka 2018.
Kauli hiyo aliisema wakati akitoa maelekezo ya ujazaji wa fomu za uteuzi kwa Wagombea waliofika kwa nyakati tofauti katika Afisi ya Tume ya Uchaguzi Maisara kwa ajili ya kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kwa nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya vyama vyao.
Mwenyekiti huyo alisema ili mtu ateuliwe na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kuwa mgombea wa kiti cha Urais, atalazimika kuwa na sifa kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Uchaguzi inavyo elekeza.
Alisemaa kuwa, mgombea atalazimika kujaza fomu ya tamko la maadili ya mwaka 2020 na tamko la kutojihusisha na vitendo vya rushwa na hai ya kiapo katika fomu katika fomu iliyojazwa na kutia saini na Mgombea mbele ya Jaji wa Mahakama kuu ya Zanzibar.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupatiwa fomu hizo na mwenyekiti wa ZEC wagombea hao walisema endapo watapata ridhaa ya kuteuliwa na wananchi watahakikisha wanaunga mkono juhudi za Serikali na kuendeleza yale yote mazuri yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya saba chini ya uongozi wa Dkt.Ali Mohamed Shein.
Walisema kuwa watahakikisha wanasimamia haki, kuimarisha uchumi na kuandaa mazingira mazuri ambayo yatatoa fursa kwa vijana kusoma hadi chuo kikuu bila ya malipo yoyote
Aidha, Wagombea hao waliahidi kuwa, wataendelea kushirikiana na Tume na Serikali katika kukubaliana na maelekezo ya Uchaguzi pamoja na kuridhia matokeo ya uchaduzi yatakayotangazwa na Tume ya uchaguzi ya Zanzibar na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Wagombea walio kabidhiwa fomu hizio ni pamoja na Mgombea wa chama cha ADA-TADEA Mhe. Juma Ali Khatib, Mgombea wa NLD ndugu Mfaume Khamis Hassan na Mgombea wa ADC Mhe. Hamad Rashid.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kesho tarehe 28/8/2020 Mgombea wa Uraisi kupitia chama cha ukombozi wa Umma (CHAUMA) saa 5:00 asubuhi, Chama cha Sauti ya Umma saa 5:30 asubuhi, Demokrasia Makini saa 8:30 Mchana na UPDP 8:30 Mchana wanatarajiwa kuchukua fomu za uteuzi