Na Jaala Makame Haji - ZEC.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imekamilisha mzunguko wa Ratiba ya kazi ya uandikishaji na uhakiki wa taarifa za Wapi Kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Wilaya zote kumi na moja Unguja na Pemba.

Akizungumza Ofisini kwake Maisara Zanzibar  Afisa Uandikishaji Wilaya ya Mjini SAFIA IDDI MUHAMMAD alisema kukamilika kwa ratiba ya uandikishaji kunatokana na ushirikiano mzuri wa Tume na Wadau wa Uchaguzi  kwa kukubali kufuata Sheria , kanuni, miongozo na maelekezo yanayohusiana na kazi ya uandikishaji.

Alisema, ZEC kabla ya kuanza kazi ya uandikishaji ilichukuwa jitihada za makusudi kuwapatia mafunzo ya utendaji watendaji wa Vituo vya Uandikishaji wakiwemo Makarani, Masheha ambao ni wakala wa Tume na Mawakala wa Vyama vya Siasa jambo ambalo limeifanya kazi hiyo kufanyika katika hali ya amani na utulivu.

 

Mwenyekiti bodi ya Shirika la Utangazaji Zanzibar ZBC mama Mahfoudha Aley Hamid akiwa katika kituo kuhakiki taarifa zake (picha Maktaba ZEC).

Bi Safia aliongeza kwa kusema kuwa Zoezi la uandikishaji lilifanyika katika hali ya amani na utulivu ambapo wananchi wote waliofika katika vituo waliweza kupatiwa huduma hata hivyo, Tume ilizipatia ufumbuzi hapo hapo changamoto zilizojitokeza na hakukuwa na changamoto kubwa ambayo  ingeweza kukwamisha zoezi hilo.

Mawakala wa vyama vya Siasa walieleza kuridhika kwao na uendeshaji wa zoezi la uandikishaji na uhakiki wa taarifa za wapiga kura kwa kuwa zoezi hilo lilikuwa linachukuwa muda mfupi wa wastani dakika moja mpaka mbili kwa mtu mmoja ambaye anahudumiwa kituoni.

Mawakala hao wameishukuru Tume kwa mpango wao huo wa kubadilisha mfumo wa uandikishaji ambao unaendesha zoezi kwa haraka zaidi.

Zoezi la uandikishaji na uhakiki wa taarifa za Wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura lilianza tarehe 18/1/2020 Wilaya ya Micheweni na Kumalizika tarehe 03/2/2020 Wilaya ya Mkoani kwa Upande wa Pemba na kwa Upande wa Unguja zoezi hilo lilianza tarehe 15/2/2020 Wilaya ya Kaskazini “A” na kumalizika tarehe 15/3/2020 Wilaya ya Mjini.

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii