Na Jaala Makame Haji- ZEC

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC imekabidhiwa Karatasi za Kura kutoka kwa wakala wa Serikali wa Uchapaji Zanzibar ambaye ni Mzabuni wa Karatasi hizo.

Makabidhiano hayo yalifanyika katika eneo la ghala kuu la Tume Kikwajuni Zanzibar ambayo yameshuhudiwa na wadau wa Uchaguzi kutoka vyama vya siasa, wajumbe na watendaji pamoja na waandishi wa habari.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Mkurugenzi wa Uchaguzi Thabit Idarous Faina alisema kwa kuzingatia  Sheria ya Ununuzi na uondoshaji wa mali za Umma nambar 11 ya mwaka 2016 kifungu cha 71(3)(b) Tume iliwaorodhesha wazabuni watatu ambao waliwasilisha wasifu na vielelezo vyao vya kazi mbali mbali walizofanya.

Aidha, Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa mchakato wa upatikanaji wa Karatasi za Kura kwa Uchaguzi Mkuu 2020 umefanikiwa baada ya Tume kupitia hatua mbali mbali za upatikanaji wa mzabuni wa uchapishaji wa Karatasi hizo.

Mkurugenzi Faina aliwataja wazabuni waliowasilisha maombi yao kuwa ni Al ghurair printing and Publishing- Plant and Equipment list kutoka Dubai, Uniprint ado hirt and carte Pty ltd kutoka Afrika Kusini na wakala wa Serikali wa Uchapaji Zanzibar.

Hata hivyo, Bw. Faina aliongeza kusema kuwa, Tume ya Uchaguzi baada ya kufanya uchambuzi wa kina kuhusu uwezo wa kila mzabuni na kwa kuzingatia mahitaji yanayotakiwa Tume ilimchagua Wakala wa Serikali wa Uchapaji Zanzibar kuwa mzabuni wa karatasi za Kura.

Akibainisha vigezo walivyotumia kumpata mzabuni huyo Mkurugenzi Faina alithibitisha kuwa Tume ilitumia kiasi cha Shilingi Milioni Mia nane na sabiini na Tisa, laki Tisa na thelathini elfu (879,930,000/=) wakati bajeti ya Tume ya Uchaguzi ya Uchapishaji ilikuwa Bilioni Moja na nusu (1.5)

Karatasi zilizokabidhiwa ni pamoja na karatasi za urais, uwakilishi na Udiwani ambapo jumla ya shiling milioni mia nane na sabiini na tisa laki tisa na thelethini elfu zimetumika kuchapishia karatasi hizo wakati bajeti ya hapo awali kuchapishia karatasi hizo ilikuwa ni bilioni moja nukta tano.

Wakizungumza baada ya hafla ya makabidhiano hayo wadau wa Uchaguzi waliipongeza Tume ya Uchaguzi kwa kutumia Mzabuni wa ndani ambaye alitumia bajeti ndogo ya fedha badala ya kutumia wazabuni wa ndani ambao wangeweza kutumia kiasi kikubwa cha fedha.

 Wadau hao ambao pia walikuwa ni shuhuda wa makabidhiano ya karatasi za kura walisema ZEC wamefanikiwa sana kwa kuweza kuzingatia mahitaji ya Makundi ya Watu wenye Ulemavu kwa kuwa wameweza kuchapasha kifaa cha kupigia Kura watu wasioona bila Msaada (tactile ballot folder)

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii