Na Jaala Makame Haji - ZEC

Tume ya uchaguzi ya Zanzibar imewahakikishia wananchi kuwa itazifanyia kazi changamoto zinazojitokeza katika zoezi la uandikishaji na uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura baada ya kukamilisha zoezi hilo.

Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu HAMID MAHMOUD HAMID aliyasema hayo huko Skuli ya Kiembe Samaki baada ya kuhakiki taarifa zake katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Alisema Tume, inafahamu kuwa kuna baadhi ya Watu hawajapata fursa ya kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao kwa sababu ya kukosa vitambulisho vipya vya Mzanzibari Mkaazi kutokana na sababu mbalimbali hivyo, Tume itafanya tathmini na kutafuta njia itakayowasaidia ambao walikosa kujiandikisha baada ya kuijua idadi yao ili kila mwenye sifa aweze kuwemo katika Daftari na kushiriki katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe Jaji Mkuu mstaafu HAMID MAHMOUD HAMID (kulia) akiwa katika kituo cha Skuli ya Kiembe Samaki kuhakiki taarifa zake katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura leo tarehe 28/2/2020 (Picha na Jaala Makame Haji-ZEC)

Naye Makamo Mwenyekiti wa chama cha ADA- TADEA JUMA ALI KHATIB baada ya kuhakiki taarifa zake katika kituo cha Skuli ya Kiembe Samaki alisema ushiriki wa wananchi katika zoezi hilo unatokana na Mwamko wa Wazanzibar kufahamu haki na wajibu wao katika masuala ya kiuchaguzi ambapo aliwaomba Tume ya Uchaguzi kuendelea kuwapatia wananchi elimu ya Wapiga Kura ambayo itawasaidia katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi mkuu.

Makamo Mwenyekiti wa chama cha ADA-TADEA Mhe. JUMA ALI KHATIB akiwa katika kituo cha Skuli ya Kiembe Samaki kuhakiki taarifa zake katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura leo tarehe 28/2/2020 (Picha na Jaala Makame Haji- ZEC)

Kwa hatua nyengine Afisa uandikishaji wa Wilaya ya Mjini SAFIA IDDI MUHAMMAD wakiti akizungumza na wadau wa Uchaguzi katika kituo cha Elimu Mbadala alisema, Zoezi la uandikishaji linatarajiwa kuanza tarehe 6/3/2020 katika vituo vyote 56 ambavyo vimepangwa na Tume katika Wilaya hiyo ambapo amewataka wananchi kushiriki katika hali ya amani na utulivu.

Kwa upande wake Msaidizi Afisa uandikishaji Magharib “A” MWANAMKUU GHARIB MGENI alisema Sheria ya uchaguzi ya Zanzibar Nam. 4 ya mwaka 2018 imeweka  utaratibu mzuri wa kujiandikisha kwa kila mtu aliyetimiza sifa za kuwemo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura hivyo kila mwananchi anawajibu wa kufuata maelekezo yaliyomo katika Sheria hiyo kwa maslahi yao na taifa kwa jumla.

Zoezi la Uandikishaji na uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura linatarajiwa kumaliza tarehe 29/2/2020 kwa Wilaya ya Magharib “B” na Jimbo la Tunguu ambapo tarehe 1/3/2020 mpaka tarehe 5/3/2020 zoezi hilo litafanyika katika majimbo yaliyobakia kwa Wilaya ya Kati na Majimbo yote ya Wilaya ya Kusini.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii